|
TEKNOHAMA zinavyotumiwa na wahalifu kuhujumu na kuiba
Na Aloyce Menda
Teknolojia kama zilivyo dawa za tiba zinaweza kuwa na faida kubwa kwa binadamu lakini pia zinaweza kuleta madhara zikitumiwa vibaya.
Karibu kila teknolojia iliyowahi kugunduliwa duniani imeleta faida na madhara kiasi fulani kwa binadamu.
Teknolojia za Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) kwa mfano ni mojawapo ya vitu vyenye faida kubwa sana kwa binadamu katika shughuli zote za maendeleo ya kiuchumi na kijamii, lakini zimeshaanza kutumiwa vibaya na wahalifu na kuleta madhara makubwa kwa baadhi ya watumiaji.
Hakuna mtu mwenye akili timamu atakayekana ukweli kwamba teknolojia kama ndege za kubeba abiria ni muhimu sana kwa maisha ya binadamu wa leo. Lakini kama walivyofanya magaidi wa Al-Qaeda, yalipoteka ndege za abiria na kuzibamiza kama mabomu kwenye majengo katika miji ya Marekani Septemba 11, 2001, ndivyo hivyo wanavyofanya wahalifu wanaotumia TEKNOHAMA kuhujumu na kuiba.
Miongoni mwa TEKNOHAMA imebainika kwamba Mtandao wa Intanet ndio wenye mianya mingi zaidi inayoweza kutumiwa na wahalifu kuhujumu au kuiba. Kadri Intanet inavyozidi kuboreshwa na kusambaa duniani ndivyo hivyo hivyo wahalifu nao wanavyozidi kuongezeka na kugundua mbinu mpya za uhalifu.
Wahalifu wengi wanaotumia Intanet ni wasomi wa TEKNOHAMA ambao ni werevu sana lakini wamekosa ajira au hawapendi ajira za ujira mdogo. Hawa wanafahamu vizuri sana nguvu za TEKNOHAMA katika kuleta maendeleo na pia wanajua jinsi ya kutumia TEKNOHAMA kwa njia mbalimbali kuboresha biashara na huduma za kijamii. Lakini kwa sababu akili na dhamira zao zimeshachafuliwa kwa nguvu na hila za shetani hawapendi kutumia ujuzi wao kwa manufaa ya binadamu.
Huko Marekani ambako ndio Mtandao wa Intanet uligunguliwa na kuanza kutumiwa, Serikali ya huko imeshaanza mikakaki kabambe kupambana na wahalifu wa aina hii katika nchi mbalimbali.
Vita dhidi ya Ugaidi duniani iliyotangazwa na Marekani na kuungwa mkono na washirika wake baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001 imefanya ulinzi kuongezwa sana katika sekta zote zinazotumia au kujihusisha na TEKNOHAMA.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Bwana Donald Rumsfeld alisema uhalifu dhidi ya mifumo ya kiteknolojia hususan inayohusu TEKNOHAMA imegawanyika katika makundi matatu. Kundi la kwanza ni la uhalifu unaofahamika vizuri ambao unaweza kukwamisha mifumo ya mawasiliamo katika sekta za usafirishaji wa anga, miundombinu ya nishati, simu na huduma nyeti ya kijamii.
Kundi la pili ni uhalifu usiofahamika vizuri na watu wengi lakini unaoweza kutokea kwa mujibu wa tasmini za wataalamu. Katika kundi hili wahalifu wanaibia watu, makampuni, mashirika au mabenki kwa njia ya TEKNOHAMA nap engine watu wanaoibiwa wanashindwa kujua au wanadharau kwa sababu wezi wanaiba kidogo kidogo kwenye akaunti na kwa kuwa wanaibia wengi pesa wapatazo kwa ujumla ni nyingi.
Kundi la tatu ni la uhalifu usiofahamika na watu wengi wala wataalamu lakini unaweza kutokea kutokana na mianya iliyopo katika mifumo ya TEKNOHAMA.. Kwa mujibu wa Rumsfeld uhalifu huu unafanywa na magenge ya wahalifu wanaojua vizuri TEKNOHAMA lakini hawatumii ujuzi wao kujenga bali kwa kufanya uhalifu. Wahalifu wa namna hii wanaweza hata kufanya hujuma kwa ajili ya kujifurahisha tu bila kupata faida yoyote. Pia wanaweza kutumiwa na magaidi kuhujumu uchumi kwa kuharibu mifumo ya mawasilaino au huduma nyeti zinazoendeshwa kwa kutegemea TEKNOHAMA.
UHALIFU UNAVYOFANYWA
Wahalifu wanaotumia Intanet ni werevu sana na wna mbinu nyingi za kitaalamu za kuhujumu au kuiba. Kampuni ya Mi2g (ya Marekani) inayojihusisha na usalama wa kompyuta inakadiria kwamba madhara yanaoyotokana na uovu wa wahalifu wanaotumia Intanet yaliweza kufikia Dola za Kimarekani bilioni 37 hadi 45 kwa mwaka 2002 peke yake. Mwaka jana (2003) yaliweza kufikia dola bilioni 135 na ilikadiriwa kuongezeka mara tatu zaidi 2005.
Mi2g inasema katika moja ya ripoti zake za utafiti kwamba, wahalifu wanaleta madhara kila sehemu na sio tu katika nchi zilizoendelea. Huko Brazil kwa mfano Mi2g inasema makampuni makubwa ya biashara yameshapata hasara sana kutokana na wahalifu hawa. Mwaka 2003 asilimia 77 ya wakuu wa makampuni hayo walitoa malalamiko serikalini kuhusu wahalifu wa kutumia Intanet. Hilo lilikuwa ni ongezeko la asilimia 45 kutoka katika idadi ya malalamiko yaliyotolewa 2002. Huko Urusi nako, watumiaji wa Intanet waliibiwa kiasi cha takriban dola bilioni sita mwaka 2002, kiasi ambacho ni mara tatu zaidi ya kile cha mwaka 2001.
Uhalifu wa kutumia Intanet unaweza kuwa ni kazi ya magaidi wa kimataifa kama Al-Qeada, lakini wataalamu wa usalama wanasema toka yalipotokea mashambulizi ya Al-Qeada Septemba 11, 2001 huko Marekani, uhalifu huo unazidi kukua licha ya vyombo vya usalama kuongeza juhudi na maarifa. Hii inathibitisha kwamba wahalifu wengi wanaotumia Intanet sio magaidi wa kimataifa bali ni wezi tu wenye elimu bora isiyotumika.
BARUA ZA UTAPELI
Katika mawasiliano ya taasisi mbalimbali, mtumiaji wa Intanet anaweza kutoa anwani yake kwa watu mbalimbali hata asio wajua. Hatari yake ni kwamba matapeli wanaweza kupata anwani hiyo na kutuma kwako taarifa usizozihitaji. Baadhi ya taarifa zinaweza kuwa za utapeli uliopangiliwa kwa maneno mazuri yenye kutamanisha.
Barua moja kwa mfano inasema umebahatika kushinda bahati nasibu ambayo hujawahi kushiriki. Inasema anwani yako ya barua pepe (e-mail) imechaguliwa kwa kompyuta kutoka katika orodha ndefu ya watumiaji wa Intanet. Tena unaambiwa anwani hiyo ikashindanishwa bila wewe mwenyewe kufahamu na ukatokea kuwa mshindi wa kwanza unaestahili kitita cha Dola za Kimarekani milioni 25!
Tapeli anaongeza katika waraka wake kwamba bahati nasibu yenyewe imefanyika huko Geneva, Uswisi na kampuni fulani. Anaitaja jina kabisa na kutoa anwani yake ya posta, mtaa ofisi zake zilipo na namba zake za simu. Mwisho wa waraka tapeli anakushauri ufanye haraka kuwasiliana naye ili akuelekeze jinsi ya kuchukua kitita chako. Anakuomba kwamba ufanya waraka huo kuwa siri kubwa kwani fedha hiyo inaweza kuibiwa na 'wajanja' watakautumia anwani yake ya barua pepe kudai wao ndio washindi halali.
Kwa kutamanishwa namna hiyo mtu mwenye akili timamu anaweza kujiuliza maswali kadhaa. Je, anayekuletea waraka huu anategemea kupata faida gani? Je, yeye ni tajiri sana na hapende fedha? Je, amefahamu vipi kwamba wewe umeshinda bahati nasibu hiyo.
Ukiamua kujibu waraka wake atakuomba umpatie namba yako ya simu na kwamba atahitaji kufahamu kama una akaunti katika benki na kama iko sehemu gani. Swali hili ataliuliza kwa ujanja sana kwani huo ndio mtego wake halisi. Atasema anataka kufahamu akaunti yake ili aweze kutuma fedha kampuni iliyochezesha bahati nasibu hiyo iweze kukutumia fedha zako ulizoshinda.
Ukiwasliana kwa simu na kampuni aliyotaja utapata jibu hilo hilo, kwamba tuma namba yako ya akaunti, benki iliyopo, anwani yake nakadhalika. Ukifanya kosa la kutuma hiyo namba basi umeshaingia kwenye mtego. Matapeli hawa watafanya ujanja wanaojua hadi wafahamu katika akaunti hiyo kuna fedha kiasi gani na kisha wataziiba kwa njia za utapeli wa hali ya juu.
Matapeli wa namna hii wapo wengi na wanasadikiwa kuwa asili yao ni Nigeria. Wnatuma barua za aina nyingi zinazofanana na hiyo Nyingine zinatoa taarifa kuhusu fedha za viongozi walioibia nchi zao huko Afrika kama akina Mabotu Seseko, Sani Abacha, Macias Nguema, Jonas Savimbi na kwamba fedha hizo zimewekwa katika hazina ambayo imefichwa sehemu fulani huko Ulaya kama urithi. Wanapotaja hazina hizo huwa ni fedha nyingi sana na wanajifanya wao ni ndugu au watu waliokuwa karibu sana na viongozi hao ambao ni marehemu.
Sasa hatimaye waraka huhitimishwa kwa ombi la ushirikiano na wewe ili kwa pamoja muweze kutumia fedha hizo na matapeli hayo. Kinachohitajiwa katika hila zote hizo ni anwani yako sahihi, namba ya simu, akaunti yako na benki ilipo. Wakishapata vyote hivyo wanakumaliza!
TANZANIA HAIJALAA
Kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea, Tanzania pia ipo katika hatari ya kudhurika kirahisi kutokana na uhalifu au hujuma za wahalifu wa kimataifa wanaotumia TEKNOHAMA.
Kwa kujua hilo tayari serikali kwa msaada wa wafadhili mbalimbali inasomesha wataalamu wa kuweza kutanzua na kubaini hila za kihalifu kwa njia za TEKNOHAMA.
Miongoni mwa wataalamu hao ni wanasayansi wanne kutoka Idara ya Kompyuta, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanausomea shahada za juu kabisa kuhusu kinga dhidi ya uhalifu wa kutumia TEKNOHAMA. Hao ni Respickius Casmir, Jabir Kuwe Bakari, Job Asheri Chaula na Charles Tarimo wanaosoma Chuo Kikuu cha Stockholm huko Sweden. Julai 13 mwaka huu wasomi hao walitoa mada zao katika semina juu ya kinga dhidi ya uhalifu wa TEKNOHAMA katika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) mjini Dar es Salaam. Semina hiyo ilitayarishwa mahsusi kwa ajili ya wataalamu wa TEKNOHAMA katika taasisi na kampuni kadhaa za mjini Dar es Salaam.
Walitoa tahadhari kwa washiriki wa semina hiyo kwamba kama suala la kinga dhidi ya uhalifu wa kutumia teknojia hizo za kisasa halitachukuliwa kwa uzito na menejimenti zao basi hi heri waache matumizi ya teknolojia hizo au watarajie hasara ya kishindo muda wowote. Walisema 'mabomu' hatari yanayotumwa kwa njia za elektronik yanaweza kuharibu mifumo ya Intanet na kompyuta, na vifaa mbalimbali vya TEKNOHAMA. Miongoni mwa mabomu hayo ni virus kama kile hatari kinachoitwa trojan horse, taarifa za uongo na wizi wa udangayifu kwa kutumia kadi bandia za kibenki zinafanya kazi kwa njia ya elektronik.
Walishauri kila mtaalamu wa mifumo ya kompyuta katika seka yoyote afanye uchambuzi kubaini mianya iliyopo inayoweza kupenyeza uhalifu wa namna hiyo kirahisi. Mianya ipo mingi kwa mujibu wa wataalamu hao na wahalifu wana mbinu nyingi lakini hiyo haina maana kwamba hawawezekani.
Respickius Casmir aliwaambia wanasemina kwamba ulinzi unatakiwa kulenga katika kuzuia uharibifu wa vifaa na pia kuvuja kwa taarifa muhimu za siri zinazohifadhiwa kwa njia za elektronik katika mifumo ya kompyuta za taasisi yoyote iwe benki, jeshi, idara ya serikali au kampuni ya biashara. Wafanyakazi wanaotumia TEKNOHAMA katika sehemu zote muhimu ni lazima wafundishwe na kuzingatia ulinzi wa vifaa na taarifa nyeti.
Alisema wahalifu wengine wanapenda tu kuhujumu vifaa au taarifa za taasisi fulani hata kama kwa kufanya hivyo hawapati faida yoyote. Hata hivyo wasomi hao walitahadharisha kwamba kwa kuzidisha sana tahadhari na mbinu za kinga haina maana kwamba ndio lazima taasisi itakuwa salama. Kitu muhimu ni kwa menejimenti kuzingatia kwamba uhalifu wa aina hiyo upo na kwamba wakati wowote kunaweza kutokea shamulio.
MWISHO
Posted By:
ALOYCE MENDA
|